MAMENEJA WA TANESCO NCHI NZIMA KUFUTWA KAZI ENDAPO WATASHINDWA JAMBO HILI
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo ameagiza mameneja wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO),
watakaoshindwa kutekeleza maagizo ya wizara hiyo, waondolewe kazini
ifikapo Machi mosi mwaka huu.

Alisema hayo wakati wa kikao chake na
watendaji wa Tanesco na taasisi nyingine zilizo chini ya wizara hiyo,
kilichofanyika katika kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera.
Profesa Muhongo alitaja maagizo hayo
kuwa ni kuunganisha huduma kwa wateja wengi, kuwa na makusanyo makubwa
ya ankara za umeme, kupunguza manung’uniko ya wananchi katika huduma za
umeme na uboreshaji wa mawasiliano kati ya Shirika hilo na wananchi.
“Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco,
ifikapo Machi mosi mwaka huu atatuthibitishia kama mameneja hawa
wataendelea na majukumu haya wanayosimamia ama la, na hii itatokana na
ufanisi wa utendaji katika majukumu tuliyowapangia,” alisema Profesa
Muhongo.
Mbali na mameneja hao, Profesa Muhongo
ameagiza Kitengo cha Uwekezaji cha Tanesco, kama hakitakuwa na miradi
mipya ya umeme ifikapo Aprili 2 mwaka huu, watendaji katika Ofisi hiyo
waondolewe katika nafasi hiyo kwa kushindwa kutimiza majukumu yao
ipasavyo.
“Hapa hatuna mzaha kwani mahitaji ya
umeme ni makubwa na tuna miradi mingi ya usambazaji umeme kwa wananchi
ikiwemo miradi ya Rea (Wakala wa Umeme Vijijini).
“Wananchi wanahitaji umeme kwa
matumizi ya majumbani na kuanzisha viwanda vidogo, sasa bila miradi
mipya ya umeme, tutashindwa kusambaza umeme kwa wananchi hawa kwa kuwa
kiasi cha umeme tulichokuwa nacho sasa bado hakitoshi,” alisema Profesa Muhongo.
No comments:
Post a Comment
Comment here