WAZIRI MKUU MAJALIWA AIBUKIA BANDARI YA TANGA
TANGA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amefanya
ziara ya kushitukiza ya kukagua Bandari ya Tanga na kumtaka Mkuu wa
Bandari hiyo (Port Master), Henry Arika ampelekee maelezo kuhusu
ukiukwaji wa ununuzi wa tishari ifikapo leo saa 6 mchana.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili Tanga jana
mchana kushiriki maziko ya Mzee Ally Mwalimu Makwaya, ambaye ni baba
mzazi wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu, aliamua kuzuru bandari hiyo kabla ya kuelekea uwanja wa
ndege akiwa njiani kurejea Dar es Salaam.
Katika
ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikataa kuingia ofisini (bandarini) na
akataka apelekwe mahali tishari tatu za bandari hiyo zilipo.
Katika maswali aliyoulizwa na Waziri
Mkuu, Arika alikiri kuwa matishari hayo hayafanyi kazi kama inavyotakiwa
kwa sababu yanasubiri kusukumwa na tugboat (meli ndogo).
“Nataka kesho saa 6 mchana uniletee
barua yenye maelezo ni kwa nini mlinunua tishari tatu ndogo badala ya
mbili kubwa, wakati mnajua Serikali ilitenga Dola za Marekani milioni
10.113, kwa ajili ya kununua tishari mbili zenye uwezo wa kujiendesha
zenyewe.
“Nataka maelezo ni kwa nini
mlizinunua tangu mwaka 2011 lakini zimekaa bila kufanya kazi hadi
Novemba mwaka jana? Na kwa nini mnaendelea kutumia fedha za Serikali kwa
kukodisha tishari kutoka Mombasa, badala ya kutengeneza za kwenu au
kufundisha vijana wa Kitanzania? Kwani tunao wahitimu wangapi wa fani
hii?” Alihoji Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema anazo
taarifa kwamba moja ya tishari lilidondoka baharini, wakaenda kutafuta
huko na kulivuta hadi pwani ndiyo maana yameshindwa kufanya kazi
inavyotakiwa.
Katika majibu yake, Arika alisema wao waliagiza tishari hizo kupitia ofisi ya Bandari Makao Makuu ambayo iko Dar es Salaam.
“Pia wakati zinaagizwa sikuwepo hapa Tanga. Nimekuja mwishoni mwa mwaka jana,” alisema Mkuu huyo wa Bandari ambaye inaelezwa alitokea Mamlaka ya Bandari Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza awaite watu wa Mamlaka
ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Bandari na Jeshi la Polisi wakae na kutafuta
mbinu za kudhibiti njia za panya zinazotumika kupitisha sukari ya
magendo.
“Mkuu wa Mkoa simamia hawa watu,
msaidiane kudhibiti uingizaji wa sukari kwa njia za panya. Kuna majahazi
yanaleta sukari kutoka Brazil. “Mheshimiwa Rais amepiga marufuku
uingizaji wa sukari kutoka nje ili viwanda vyetu vya ndani viongeze
uzalishaji. Dhibitini bandari zote ndogondogo hadi Pangani,” aliagiza
Waziri Mkuu.
Alisema changamoto inayoikabili
Serikali ni kwamba hata Shirika la Viwango Tanzania (TBS) au Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA) hawawezi kukagua sukari hizo na hazijulikani
ubora wake licha ya kuwa zinafika kwa walaji.
No comments:
Post a Comment
Comment here