Sunday, March 27, 2016

MWANZA: MTOTO MWENYE UMRI WA SIKU 1 AIBWA HOSPITALINI

Mtoto wa siku moja ameibwa katika mazingira ya kutatanisha katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, akiwa pembeni mwa mama yake aliyekuwa amelala, mwenye umri wa miaka 16.

Akizungumzia uporaji huo jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha, amesema aliyepora mtoto huyo aliingia ndani ya wodi ya wazazi ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando, akiwa amejifunga ushungi.

 

“Alipoingia wodini alikuta mama wa mtoto amesinzia akiwa peke yake wodini, ndipo akamuiba mtoto wake wa kike mwenye umri wa siku moja na kuondoka naye kwenda kusikojulikana,” alisema.

Kwa mujibu wa Kamanda Kamugisha, Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa tukio hilo kwa kuhoji wauguzi, walinzi na wazazi waliokuwa wamelazwa wodini hapo.

Katika hatua nyingine, Kamanda Kamugisha amesema Jeshi la Polisi mkoani humo, litaanza kufanya uhakiki wa silaha kuanzia Aprili mosi hadi Juni 30 mwaka huu, katika ofisi za makamanda wa Polisi wa wilaya zote za Mkoa wa Mwanza.

 

No comments:

Post a Comment

Comment here