Tuesday, June 7, 2016

MAREKANI KUIPATIA TANZANIA DOLA MILIONI 800

MAREKANI

Uthibitisho wa kutolewa kwa msaada huo, umetangazwa na Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress aliyekutana na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli katika Ikulu ya Dar es Salaam jana.

Balozi Childress alisema kutolewa kwa fedha hizo ni uthibitisho kuwa kutotolewa kwa fedha za awamu ya pili ya Mradi wa Changamoto za Milenia (MCC-2), hakujaondoa uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na Marekani, ikiwemo utoaji wa misaada ya maendeleo.

“Tumezungumza mambo kadhaa, na wiki hii Tanzania na Marekani kupitia shirika letu la misaada la USAID tunatarajia kutiliana saini mkataba wa zaidi ya dola milioni 400 kwa ajili ya mwaka ujao, pia tumezungumza kuwa kutakuwa na dola milioni 800 zitakazotolewa na Marekani kwa ajili ya miradi mbalimbali na hii haihusiani na MCC,” alisema Balozi Childress muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo na Rais Magufuli.

“Ukweli ni kwamba tunayo mengi ya kufanya pamoja katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu na kilimo na tutafanya kila juhudi kuhakikisha haya yanafanikiwa,” alisema. Naye Rais Magufuli alisema Serikali yake ya Awamu ya Tano, itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na Marekani na kwamba fedha za msaada kutoka Marekani ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania.

 

No comments:

Post a Comment

Comment here