Tuesday, June 7, 2016

KUTOKA BUNGENI:KANUNI ZA BUNGE ZALINDA POSHO ZA UPINZANI



UDHAIFU wa Kanuni za Bunge katika kufafanua mambo mbalimbali ya uendeshaji wa Bunge, umeelezwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kuwa unatakiwa kurekebishwa ili kutoa nafasi ya Kiti cha Spika kutoa uamuzi dhidi ya vitendo visivyokubalika vinavyoendelea ndani ya Bunge.Amesema hayo jana alipokuwa akitoa majibu wa muongozo alioombwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) kuhusu uhalali wa posho wanazolipwa wabunge wa Kambi ya Upinzani, ambao wamekuwa wakiingia bungeni kusaini posho na kwenda kupumzika.

Dk Tulia alisema tangu Mei 30, mwaka huu, wabunge hao wamekuwa wakiingia bungeni kusaini posho na kuondoka kwenda kupumzika, jambo lililosababisha Dk Mwakyembe kuomba muongozo kama malipo hayo ni haki kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya Katiba ya 23.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 23, ibara ndogo ya kwanza na ya pili; “Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa za kazi wanayoifanya.

Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki.” Akitoa muongozo wake kama malipo hayo ya posho ni halali kwa mujibu wa Katiba au la, Naibu Spika alisema ametumia uamuzi wa Kiti cha Spika uliotolewa Aprili 27, 2016 kuhusu muongozo kama huo.

No comments:

Post a Comment

Comment here