KUHUSU KIFO CHA SHABIKI HUYU WA SOKA
BAADA ya jana jioni kutokea kifo cha
shabiki wa Azam, Emmanuel Machibe, kwenye Uwanja wa Azam Complex
Chamazi, uongozi wa timu hiyo umetokeza na kusema wanajisikia unyonge na
kifo cha shabiki huyo.
Machibe, aliyekwenda uwanjani hapo kwa
ajili ya kushuhudia mchezo wa timu yake dhidi ya Stand United, alikutana
na kifo hicho baada ya kukanyagwa na gari.
Taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa
klabu hiyo ilisema, Azam, inapenda kutuma salamu za rambirambi kwa
familia ya Machibe, kufuatia kifo cha mpendwa wao.
Taarifa hiyo ilisema Azam, imesikitishwa
na kifo cha kijana huyo na inapenda kutoa pole kwa familia, ndugu,
jamaa na marafiki pamoja na wapenzi wote soka nchini katika kipindi hiki
kigumu cha maombolezo.
“Licha ya timu yetu kupata ushindi, lakini hatukufurahishwa na
tukio la kuondokewa na mpendwa wetu Machibe ambaye ni mkazi wa Kiwalani jijini Dar es Salaam.
“Tunatoa
pole kwa Watanzania wote ambao ni wana michezo baada ya kuondokewa na
shabiki wetu Machibe, ambaye ni kati ya mashabiki bora na tunaungana na
familia ya marehemu (Machibe) kwenye kipindi hiki kigumu walichonacho” ilisema taarifa hiyo.
Machibe, anatokea katika kikundi cha ushangiliaji cha Azam kutoka Tawi la Mpira Kazi lililopo Magomeni jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
Comment here