USHINDI WA YANGA,AZAM WAMTIBUA MAYANJA
DAR ES SALAAM
KOCHA wa Simba, Jackson Mayanja,
amesema Ligi Kuu Tanzania Bara imezidi kuwa ngumu baada ya Yanga na Azam
kushinda mechi za viporo, lakini amejipa moyo nafasi ya ubingwa bado
ipo wazi.
Yanga juzi iliifunga Mwadui FC ya
Shinyanga mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Azam FC
iliifunga Mtibwa Sugar bao 1-0 Uwanja wa Manungu, Turiani.Azam
imemaliza mechi zake za viporo, ambapo imecheza mechi 24 ikiwa na
pointi 55 ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga iliyocheza mechi 23
ikiwa na pointi 56.
Yanga itamaliza mechi yake ya viporo Jumamosi dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba ndiyo inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 57 baada ya kucheza mechi 24.
Kocha Mayanja alisema ushindi wa Yanga
na Azam umezidisha ugumu kwenye ligi na sasa hawana budi kuongeza
jitihada kushinda mechi zao.
“Hakuna kupumzika, lazima kichwa kiume kujua tutafanya vipi kuwa mabingwa, ligi imezidi kuwa ngumu,” alisema.
Taji la ubingwa wa ligi ndilo pekee
lililobaki kwa Simba kulipigania baada ya kutupwa nje ya michuano ya
Kombe la Shirikisho (Kombe la FA) mwanzoni mwa wiki hii.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani
Jumapili kuikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Taifa Dar es
Salaam, mechi yenye ushindani wa hali ya juu kutokana na timu hiyo ya
Mwanza kutoa upinzani mara kwa mara inapokutana na Simba.
No comments:
Post a Comment
Comment here