UDA WAIKANA FAMILIA YA JAKAYA KIKWETE
Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Simon
Group, Robert Kisena ameeleza kusikitishwa na taarifa zisizo za kweli
zinazoihusisha familia ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na umiliki wa
Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) na kusisitiza kuwa yeye ndiye
mmiliki halali.
Kisena alidai kwa muda mrefu watu wenye
nia mbaya dhidi yake, wamekuwa wakihoji umiliki wa shirika hilo licha ya
kuonyesha vielelezo vyote. Alisema taarifa zilizosambaa hivi karibuni
zinazodai kuwa anaimiliki Uda kwa ushirikiano na Khalfan ambaye ni mtoto
wa Kikwete hazina ukweli.
Alidai
kuwa Kampuni ya Simon Group ambayo ilisajiliwa Mwanza 2007, inamilikiwa
na watu wanane wa familia ya Kisena isipokuwa Profesa Juma Kapuya
ambaye ana asilimia tano ya hisa kwenye kampuni hiyo.
“Kampuni
hii inamilikiwa na watu wanane, hata mkisoma hizi nyaraka mtaona majina
ya watu hao ambao ni mimi, wanangu; Simon, Gloria, Kulwa na George;
mdogo wangu William Kisena, mama yangu Modesta Pole na Profesa Kapuya.
“Hakuna jina la Khalfan Kikwete hapa, sijui hizo taarifa watu wanazitoa wapi,” alihoji Kisena huku akionyesha vielelezo.
Alisema
hata wakati kampuni hiyo inaanzishwa, Khalfan alikuwa mtoto mdogo
ambaye asingeweza kumiliki kampuni hiyo ambayo inakua kwa kasi.
Kisena alidai taarifa hizo za uongo
zinaenezwa na watu ambao ni washindani wake kibiashara na wengine ni
maadui wa kisiasa wa Kikwete.
Alisema yeye ni kada wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) na amekuwa hivyo siku zote, lakini hajihusishi na siasa
bali anafanya biashara.
“Kama kuna wanaoichafua familia ya Kikwete waache kuniunganisha na mimi, sifanyi siasa.
“Na kama kuna wanaonichafua kibiashara basi waache kuiingiza familia ya Kikwete, wapambane na mimi kwenye biashara,” alisema Kisena.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alisema
kampuni yake ya Uda RT ndiyo itakayoendesha mradi wa mabasi yaendayo
kasi na kuwa nauli zilizopendekezwa zilitokana na tathmini ya gharama
halisi za uendeshaji wa mradi huo.
Alisema baadhi ya vitu vilivyowafanya wapendekeze nauli hizo kuanzia Sh700 mpaka Sh1,200 ni pamoja na kulipia barabara za Dart.
Pia, alisema mabasi hayo yatakuwa hayakai vituoni kwa hiyo huenda wakati mwingine yatakuwa yanatembea bila abiria.
“Sababu
hizo ndiyo zimetufanya tupendekeze nauli hizo, lakini tuko kwenye
mazungumzo na Serikali ili waondoe malipo ya barabara ili nauli
ipungue.Mazungumzo yanaenda vizuri, ninaamini nauli zitapungua,” alisema.
Kisena alisema ifikapo Machi, mwaka huu,
Kampuni ya Uda itaorodheshwa kwenye Soko la Hisa ili wananchi waweze
kumiliki wenyewe kampuni hiyo.
Alisema wanaendelea kufanya mipango kwa ajili ya kuuza asilimia 70 ya hisa kwa wananchi wote.
No comments:
Post a Comment
Comment here